Kabla ya matibabu yoyote, daktari mwenye ujuzi wa tiba, atachunguza kwa
kuangalia sehemu ya njia ya haja kubwa na kuona kwa macho hali halisi
ilivyo. Baada ya hapo daktari anaweza kufanya kipimo kwa kutumia kidole
cha shahada. Kidole hiki kikiwa ndani ya mpira wa kuvaa mikononi,
kinaweza kulainishwa kwa vilainishi salama na kuingizwa katika njia ya
puru ili kubaini hali ya uvimbe.
Daktari pia anaweza kutumia kipimo cha kutazama moja kwa moja katika
njia ya haja kubwa kijulikanacho kwa jina la Proctoscopy au kipimo cha
kutazama ndani ya utumbo mpana, Sigmoidoscope. Kipimo cha maabara cha
kubaini damu iliyofichika; faecal occult blood test, nacho kinaweza
kufanyika pale bawasiri daraja la kwanza inapokuwa ndani na inapokuwa
vigumu kuibaini kwa kipimo cha kidole au proktoskopi.
Matibabu ya bawasiri kimsingi hutegemea dalili, hali na hatua ya
ugonjwa. Kwa kawaida tiba ya awali ni kurekebisha mfumo wa maisha na
mtindo wa kula. Mgonjwa hushauriwa kunywa maji mengi na kula vyakula
vitakavyolainisha kinyesi kila siku. Vyakula hivyo ni kama vile matunda
na mbogamboga kwa wingi, vyakula asili visivyo vya kukoboa, aepuke
chumvi nyingi na pombe.
Mara nyingi mgonjwa hutibiwa kwa njia za kawaida zisizohusisha tiba kwa
njia ya upasuaji. Mgonjwa mwenye kinyama au kivimbe kinachojitokeza nje,
ataelekezwa jinsi ya kukalisha eneo la haja kubwa katika maji ya
vuguvugu kwa muda wa dakika 15. Atatakiwa kufanya hivyo mara nyingi
kadiri iwezekanavyo hasa kila baada ya kujisaidia.
Mgonjwa pia anaweza kupewa dawa za kupaka kwenye uvimbe ulioko katika
njia ya haja kubwa au vidonge vya kuingiza ndani ya tundu la njia ya
haja kubwa. Tiba hizi zitasaidia kupunguza uvimbe na maumivu anayoyapata
mgonjwa wa bawasiri hasa wakati wa kujisaidia haja kubwa.
Kama maumivu yatazidi, tiba rahisi iitwayo ‘Rubber band ligation’
inaweza kufanyika kwa bawasiri iliyoko ndani ya puru, yaani pale mishipa
inapokuwa haijajitokeza nje. Bawasiri daraja la kwanza na la pili. Hapa
mishipa hufungwa na rubber band ili kuzuia damu kwenda kwenye eneo
lililoathirika. Tiba nyingine ni ile ya kuunguza na kufunga uvimbe wa
kinyama kwa kifaa maalumu (laser therapy).
Kama uvimbe wa mishipa ya vena ni mkubwa sana na unajitokeza sana nje ya
puru (bawasiri daraja la 3 na 4), upasuaji unaweza kufanyika na hapa
kinyama hukatwa na kuondolewa, kisha damu inayotoka hudhibitiwa
kitaalamu. Tiba hii kitaalamu hujulikana kwa jina la haemorrhoidectomy.
Katika hospitali kubwa, aina nyingine ya upasuaji wa kisasa zaidi
inaweza kufanyika pia. Tiba hii kwa jina la kitaalamu hujulikana kama
Doppler-guided Haemorrhoidal Artery Ligation Operation (HALO) na wengine
hupendelea kuiita Transanal Hemorrhoidal
Dearterialization-Hemorrhoidectomy (THD).
Tiba hii ya upasuaji hufanyika bila kukata kinyama na bila kutumia dawa
ya usingizi ingawa ganzi inatumika. Ni tiba ambayo haisababishi maumivu
na mgonjwa anaweza kuendelea na shughuli zake baada ya saa 48 tokea
kipindi cha kufanyiwa upasuaji.
Katika tiba hii, mishipa yote inayojitokeza nje, haikatwi bali
inarudishwa ndani ya puru na kushonwa kwa nyuzi zinazoyeyuka zenyewe ili
ijishikize kwenye misuli ya ndani ya haja kubwa na mishipa yote
inayopeleka damu katika kinyama kinachovimba, hufungwa.
Utafiti wa miaka 10 wa Pravin J. Gupta na Surekha Kalaskar uliochapishwa
mwaka 2008 katika jarida la sayansi za tiba liitwalo ‘Annals of
Surgical Innovovation and Research’ toleo la 2(5), unabainisha kuwa
upasuaji na kushona ngozi ya tundu la haja kubwa katika maeneo matatu
ambayo kwa kawaida hutokeza bawasiri, unatoa matokeo mazuri zaidi ya
uponaji wa bawasiri.
0 comments:
Post a Comment