Hatimaye Makatibu Wakuu Walioahidiwa kupewa Kazi Nyingine wamepata kazi


Hatimaye baadhi ya makatibu wakuu walioachwa katika uteuzi wa Rais John Magufuli wamepewa barua za kuwajulisha kuwa wamepangiwa majukumu mengine mapya, imefahamika.

Desemba 30, 2015 Rais Magufuli alifanya uteuzi wa makatibu wakuu na naibu katibu wakuu 50, huku akiwaacha baadhi yao kwa maelezo kwamba wangepangiwa kazi nyingine.

Makatibu wakuu walioachwa ni Dk Donan Mmbando (Afya), Balozi Liberata Mulamula (Mambo ya Nje), Omari Chambo (Nishati na Madini), Jumanne Sagini (Tamisemi) na Joyce Mapunjo (Afrika Mashariki).

Katika uteuzi huo, aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue aliteuliwa tena kwa maelezo kwamba ameongezewa mwaka mmoja baada ya muda wake wa utumishi kukamilika. Lakini Machi 6, Balozi Sefue aliondolewa na kumpisha Balozi John Kijazi huku naye akiahidiwa kupangiwa kazi nyingine.

Akijibu maswali ya mwandishi wa gazeti hili aliyetaka kujua hatima ya makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu walioahidiwa kupangiwa kazi nyingine, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Dk Laurean Ndumbaro alisema kuwa kati ya makatibu wakuu hao wapo waliostaafu kwa mujibu wa sheria, akiwamo aliyekuwa Balozi Sefue.

Dk Ndumbaro alisema kutokana na Balozi Sefue kufikia umri wa kustaafu hajapangiwa kazi nyingine. Pia, alisema wengine waliofikia umri wa kustaafu ni Balozi Mulamula na Chambo ambao wanasubiri kama wataweza kupangiwa majukumu mengine.

“Makatibu wakuu wote wamepata barua zao, hakuna ambaye hana kazi. Wengine wanaendelea na majukumu yao, wapo waliostaafu na walioteuliwa kuwa wakuu wa mikoa,” alieleza Dk Ndumbaro.

Dk Ndumbaro hakutaka kuwataja makatibu hao na majukumu yao mapya lakini mwingine ambaye uteuzi wake ulitenguliwa ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk Shaban Mwinjaka ambaye aliwekwa kando kupisha uchunguzi kuhusu matumizi mabaya ya Sh13 bilioni kwenye Shirika la Reli Tanzania (TRL).

Kuhusu wakuu wa mikoa na wilaya, alisema nafasi zao ni za kisiasa na mikataba yao huanza pale wanapoteuliwa na hukoma pale uteuzi wao unapotenguliwa. “Mkuu wa mkoa au wilaya mkataba wake ni pale anapoteuliwa na kutenguliwa. Hawa si watumishi wa kudumu wanafanya kazi kwa mikataba na kama hatapata nafasi nyingine inakuwa basi,” alisema.

Wengine wazua mjadala

Katika hatua nyingine, watumishi waandamizi wa Serikali waliosimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali wameanza kuzua mjadala baada ya baadhi ya wasomi nchini kuwafananisha na watumishi hewa. Watumishi hao ni wale waliokumbwa na rungu la Rais Magufuli mara baada ya kuingia madarakani Novemba 5, mwaka jana pamoja na wale waliosimamishwa kazi na mawaziri na wakuu wa mikoa.

Baadhi ya watumishi hao ni viongozi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) na Bohari Kuu ya Dawa (MSD) ambao wanaendelea kulipwa huku nafasi zao zikishikiliwa na watu wengine.

Alipotakiwa kutoa ufafanuzi juu ya hatima ya wafanyakazi hao na kama wanalipwa mshahara au la, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Angela Kairuki hakuwa tayari kueleza kuhusu malipo bali alijibu kuwa kukiwa na hitaji la kutoa ufafanuzi Serikali itafanya hivyo.

“Hili suala liko wazi sielewi kwa nini mnaniuliza na mnakwenda kuandika nini. Niambieni taarifa yote mnayokwenda kuandika ndiyo nijibu,” alisema Kairuki.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), Nicholaus Mgaya ametaka iwepo sheria moja ya utumishi kwa kuwa sheria mbili zilizopo zinatoa haki tofauti kwa wafanyakazi katika malipo pale wanaposimamishwa kazi.

“Sheria moja inasema mfanyakazi alipwe mshahara wote na nyingine inataka alipwe nusu mshahara. Wapo waliosimamishwa kazi zaidi ya miaka mitano bila hatima yao kujulikana,” alisema Mgaya.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Richard Mbunda alisema wafanyakazi waliosimamishwa kazi huku wakiendelea kulipwa hawana tofauti na watumishi hewa kwa kuwa uchunguzi unaofanywa dhidi yao unachukua muda mrefu.

“Tunapoitafsiri dhana ya watumishi hewa tusisahau kuwaweka na watumishi hawa. Tunaweza kupambana na watumishi hewa wanaopewa mishahara bila kufanya kazi wakati huohuo tunatengeneza watumishi hewa wengine,” alisema.

“Inawezekana ni suala la kiutawala kwa sababu Rais bado anajipanga, lakini kama lengo letu ni kubana matumizi katika hili hatubani matumizi hata kidogo kwa kuwa mtu anasimamishwa na anachukuliwa mwingine kukaimu nafasi yake na analipwa mshahara.”

Alisema Serikali ya Awamu ya Tano yenye miezi sita tangu iingie madarakani kuna makosa inayafanya inahitaji kukumbushwa, likiwemo hilo la waliosimamishwa kazi kuendelea kulipwa. “Uchunguzi ufanyike mapema na wanaosubiri kupangiwa kazi nyingine na iwe hivyo, ukiondoa wale ambao tayari wamefikishwa mahakamani,” alisema.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (Sua), Profesa Daniel Gabagambi alisema, “Kuongoza nchi siyo kitu kidogo, kwa hiyo baadhi ya hatua ambazo zinachukuliwa inatakiwa zitathminiwe kwa muda mrefu na muda mfupi.”

Alisema watu wanaolipwa mshahara bila kufanya kazi yoyote hawajengi uchumi wowote, lakini kama wamesimamishwa huku ikitafutwa dawa ya kukomesha utumishi mbovu ni jambo la kuungwa mkono.

“Tukiwaweka kando na kuwalipa mshahara kwa muda mfupi ili tufanye uchunguzi na kuwaadhibu ni wazi kuwa tutakuwa tumetibu kidonda,” alisema Profesa Gabagambi.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Emmanuel Mallya licha ya kupongeza hatua hizo alisema mtumishi kabla ya kusimamishwa tuhuma zinazomkabili zinatakiwa kuchunguzwa kwa kina ili kujiridhisha.

“Tunajua kisheria mtu husimamishwa kazi kupisha uchunguzi na kila mmoja, yaani mwajiri na mwajiriwa wanakuwa na haki kwa mujibu wa sheria. Kila kitu kina gharama na hata katika demokrasia kuna gharama na hiyo ni moja ya gharama zake,” alieleza.

Mhadhiri wa UDSM, Dk Benson Bana alisema, “Hilo la mtumishi kusubiri uchunguzi dhidi yake kwa muda mrefu lina mashiko. Nadhani mamlaka zilizopewa kazi ya uchunguzi na kufuatilia mambo haya zifanye kazi kwa juhudi zaidi ili hatima ya watumishi ijulikane mapema.”

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Rucu), Profesa Gaudence Mpangala alisema uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili watumishi hao haupaswi kuchukua muda mrefu. “Kama uchunguzi ukionyesha tuhuma ni za kweli basi hatua za kisheria zichukuliwe na kama hakuna kitu warejeshwe kazini maana uchunguzi ukichukua muda mrefu si sahihi,” alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: