
BUNGE
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jana lilipitisha kwa kauli moja
Sheria ya Marekebisho Mbalimbali, ambayo pamoja na mambo mengine,
yamempa Jaji Mkuu mamlaka ya kuanzisha Divisheni ya Rushwa na Uhujumu
Uchumi ya Mahakama Kuu.
Kwa
mujibu wa muswada huo uliowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
George Masaju, adhabu kwa watakaokutwa na hatia zimeongezwa, huku
mahakama hiyo ikiwekewa mazingira wezeshi ili iendeshe kesi hizo kwa
haraka.
Mazingira wezeshi
Muswada
huo wa sheria ambao kwa sasa utakuwa ukisubiri Rais ausaini ili iwe
sheria kamili, umekusudia kuanzisha divisheni hiyo ya mahakama, ambayo
itakuwa na majaji wake na watumishi wake wanaojitegemea.
“Divisheni
Maalumu ya Mahakama Kuu, itakuwa na majaji pamoja na watumishi wengine,
ambao wanahusika moja kwa moja na kesi za rushwa na uhujumu uchumi tu.
“Hatua hii itawezesha kesi za makosa ya rushwa na uhujumu uchumi kusikilizwa kwa urahisi, ufanisi na kwa haraka,” alisema Masaju wakati alipokuwa akisoma muswada huo kabla ya kupitishwa na Bunge.
Hatua
hiyo ya kuwa na majaji maalumu na wafanyakazi wake, Masaju alisema
imelenga kuondoa udhaifu uliojitokeza wakati wa kushughulikia kesi za
rushwa na uhujumu uchumi, kwa kuwa majaji waliokuwa wakisikiliza
mashauri hayo, walikuwa hao hao wanaosikiliza mashauri mengine ya jinai,
madai, katiba na mengine yanayofunguliwa Mahakama Kuu.
Kwa
mujibu wa Masaju, hali hiyo ilisababisha uendeshaji wa kesi za rushwa
na uhujumu uchumi, kutokuwa na tofauti na uendeshaji na usikilizwaji wa
kesi zingine.
Mazingira
mengine wezeshi yanayotengenezwa na sheria hiyo kwa divisheni hiyo, ni
thamani ya fedha inayohusishwa na makosa hayo, kuwa inaanzia Sh bilioni
moja.
“Inapendekezwa
kuwa pale makosa ya rushwa na uhujumu uchumi yanapohusisha thamani ya
fedha, basi makosa yatakayofunguliwa katika Mahakama Kuu, Divisheni ya
Rushwa na Uhujumu Uchumi, yawe ni yale ambayo thamani yake haipungui Sh
bilioni moja,” alisema Masaju.
Lengo
la kuweka thamani hiyo ya fedha, limeelezwa kuwa ni kuiwezesha
divisheni hiyo kujikita kusikiliza makosa makubwa ya rushwa na uhujumu
uchumi, ili makosa madogo yasiyofikia thamani hiyo, yasikilizwe na
mahakama za wilaya, mahakama za hakimu mkazi na Mahakama Kuu.
Thamani
hiyo ya fedha, imetajwa pia kusaidia kuharakisha usikilizwaji wa makosa
hayo bila kuathiri ufanisi na kupunguza msongamano wa mashauri katika
divisheni hiyo.
Hata
hivyo, divisheni hiyo pia kwa mujibu wa sheria hiyo itasikiliza makosa
mengine ya rushwa na uhujumu uchumi bila kujali thamani ya fedha,
kutokana na namna makosa hayo yalivyotendeka, asili yake na ugumu wa
kuyawekea thamani ya fedha.
Pia
Mkurugenzi wa Mashitaka amepewa mamlaka ya kutoa hati ambayo itataka
mashauri mengine yatakayofunguliwa, yasikilizwe katika divisheni hiyo
kwa maslahi ya umma.
Kifungo, utaifishaji mali
“Marekebisho
mengine yanayopendekezwa… ni kwamba makosa ya rushwa na uhujumu uchumi
chini ya sheria hii iwe ni kifungo cha gerezani, kisichopungua miaka 20
na kisichozidi miaka 30 au vyote kwa pamoja na hatua nyingine za
kijinai, ikiwa ni pamoja na kutaifisha mali zilizopatikana kutokana na
makosa hayo,” alisema Masaju wakati akiwasilisha muswada huo.
Kifungo hicho kimeongezwa kutoka katika sheria ya sasa ambayo ndiyo inayorekebishwa, ambayo ilitaka kifungo kisizidi miaka 15.
Kwa
mujibu wa Masaju, maneno hayo “kifungo kisichozidi miaka 15”, yaliipa
Mahakama mamlaka ya kutoa adhabu ndogo zaidi, ilimradi tu adhabu hiyo
haizidi miaka 15, jambo lililoonekana kuwa baadhi ya adhabu zilikuwa
ndogo kuliko uzito wa makosa.
Katika
kutaifisha mali za waliokutwa na hatia, sheria hiyo imeweka masharti ya
kuzuia kutumika kwa sheria zinazohusu ufilisi au uamuzi wa kufilisi
kampuni, kwa mali ambayo inachunguzwa chini ya Sheria ya Makosa ya
Uhujumu Uchumi.
“Marekebisho
hayo yanalenga kukabili vitendo vya watu au kampuni kujifilisisha
wakati uchunguzi unapoanza dhidi yao na pia kuhakikisha kuwa mali zote
zinazohusika na kosa linalochunguzwa, au linaloendelea mahakamani,
inaendelea kuwepo hadi uchunguzi au kesi husika itakapohitimishwa,” alisema Masaju.
Hatua
hiyo imetajwa kuwa na nia ya kuiwezesha serikali kutaifisha mali hiyo,
wakati kesi husika itakapokamilika na ikathibitika kuwa ina uhusiano na
kosa la rushwa na uhujumu uchumi lililothibitishwa mahakamani.
“Kwa
ujumla hatua hii ni njia mojawapo ya kuwafanya watu waogope kutenda
makosa ya rushwa na uhujumu uchumi na pia kuhakikisha kuwa mhalifu,
hanufaiki na uhalifu alioutenda kwa kutaifisha mali zilizopatikana kwa
njia ya rushwa, ufisadi na uhujumu uchumi,” alisema.
Ulinzi wa mashahidi
Marekebisho
mengine yaliyoingia katika sheria hiyo, yanahusu ulinzi wa mashahidi,
ambapo Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), kwa kushauriana na Mkurugenzi
wa Mashitaka, wanatakiwa kuweka utaratibu wa kuhakikisha usalama wa
shahidi pamoja na familia yake.
Lengo
ni kusaidia usalama wa mashahidi wa kesi hizo, ili mashahidi wawezeshwe
kutoa ushahidi wao bila woga, kwa kuwa kesi hizo zinahusisha watu wenye
fedha na makosa yanayofanyika ni ya kupanga.
Maoni ya wabunge
Akichangia
maoni yake kuhusu muswada wa sheria hiyo, Waziri wa Sheria na Katiba,
Dk Harrison Mwakyembe, alisema tangu amekaa bungeni, hajawahi kuona
majadiliano ya kina kwenye kamati kati ya Kamati ya Bunge na serikali
ambayo yalidumu kwa wiki mbili.
Wabunge
wengine, akiwemo Hussein Bashe wa Nzega Mjini (CCM), Mbunge wa Ileje,
Janet Mbene (CCM), Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Peter Serukamba (CCM) na
Mbunge wa Muheza, Adadi Rajab (CCM), walitaka Serikali kuiwezesha
mahakama hiyo kimafunzo na kifedha, ili itekeleze wajibu wake.
0 comments:
Post a Comment