MSAJILI
wa Vyama vya Siasa Nchini, Jaji Francis Mutungi ametetea kauli ya Rais
John Magufuli kuhusu kufanya siasa wakati huu na kwamba alichotaka
kiongozi huyo wa nchi ni ushirikiano kutoka kwa wanasiasa wenzake ili
kuwaletea maendeleo wananchi.
Alisema
Rais Magufuli, katika kauli yake ile hakumaanisha kuzuia shughuli za
siasa nchini isipokuwa alieleza kuwa hatakuwa tayari kuona siasa
zinakwamisha mikakati ya kuwapelekea wananchi maendeleo yao.
Jaji
Mutungi alisema hayo Dar es Salaam jana, alipotakiwa kutoa maoni yake
kuhusu kauli ya Rais Magufuli ya kuwataka watu kuacha siasa za hovyo
hadi mwaka 2020 utakapofanyika uchaguzi mkuu mwingine, ili muda uliopo
wautumie kuijenga nchi.
“Watu
wametafsiri tofauti kauli ya Rais, lakini ni kwamba alikuwa akiomba
ushirikiano wa wanasiasa wenzake na wadau wote wa siasa kuleta
maendeleo… kwa hiyo kabla ya kukosoa kauli ni vyema ukafanya utafiti
siyo kuibeba na kuitafsiri kwa mrengo tofauti,” alisema .
Alisema
siyo kwamba Rais anapinga siasa isipokuwa anapingana na wanasiasa ambao
ni pingamizi katika kuleta maendeleo na muda wote wamejikita katika
siasa bila kuangalia namna ya kutekeleza ahadi zao kwa wananchi.
Alisema
wapo watu walioitafsiri tofauti hotuba aliyoitoa juzi Rais Magufuli,
hivyo wananchi wanapaswa kuwa watafiti na kuweka maslahi ya nchi huku
akiwataka wanasiasa kuwa wavumilivu na kutumia muda wao kutafakari jambo
kabla ya kuzungumza.
“Rais
alikuwa akijaribu kuwasihi wanasiasa kuangalia namna ya kujikita kwenye
siasa ya maendeleo ya jamii kwa ujumla na kuachana na siasa za kupinga
maendeleo,” alisema.
Alisema
dhamira ya Rais ni kuwaletea maendeleo kwa wananchi na taifa kwa ujumla
na vyama vinapaswa kufuata utaratibu wa kuwasilisha taarifa kwa msajili
na si kusubiri hadi vyombo vya habari kutoa taarifa.
Mutungi
alisema vyama vya siasa vimekuwa vikitaka demokrasia nchini, hivyo
kabla ya vyama kufikiria demokrasia kitaifa, hivyo viongozi wake waanze
kuangalia suala hilo kwenye vyama vyao na si kuimba, kwani wapo
wanaofanya ndivyo sivyo.
Alisema
mtu anapotetea jambo, kwanza anapaswa kulitekeleza kwa vitendo huku
akibainisha demokrasia kutotokea nchini endapo demokrasia ndani ya vyama
vya siasa kuwa ni shida.
Jaji
huyo alisema bado kuna kazi kubwa huku akibainisha yapo mambo mengi
yanayotokea nchini huku akitegemea ushirikiano wao na kuwataka wanasiasa
kuwekeza katika kufanya upembuzi wa mambo kabla ya kutamka au
kuyatenda.
Naye
Msajili Msaidizi, Kitengo cha gharama za Uchaguzi na Elimu kwa Umma,
Piencia Kiure alisema ni vyama vitatu tu kati ya 22 ndivyo vimewasilisha
taarifa ya gharama za Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25 mwaka jana.
Mwisho
wa kuwasilisha gharama hizo ni leo. Alivitaja vyama vilivyowasilisha
gharama za uchaguzi kuwa ni Chama Cha Mapinduzi (CCM), ACT-Wazalendo na
Chama cha Wananchi (CUF).
Alifafanua
kuwa, mgombea atakayeshindwa kuwasilisha gharama za uchaguzi
utahukumiwa kifungo kisichozidi mwaka mmoja au faini isiyozidi Sh
milioni mbili au vyote kwa pamoja.
Aidha,
chama kitakachoshindwa kuwasilisha gharama za uchaguzi katika kipindi
kilichowekwa adhabu yake ni faini isiyozidi Sh milioni tatu na
kutoruhusiwa kushiriki uchaguzi hadi watakapofanya marejesho.
0 comments:
Post a Comment