Wizara
ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano imeanza mazungumzo na Kampuni ya
MABE BRIDGE ya Uingereza kwa ajili ya kujenga barabara za juu (fly over)
saba katikati ya jiji la Dar es Salaam ili kupunguza msongamano wa
magari.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, amesema mazungumzo kuhusu ujenzi huo yako katika hatua nzuri na kwa kuanzia zitajengwa fly over nne za watembea kwa miguu na tatu za magari.
Amesema
Fly over hizo zitazojengwa zitatumia miezi mitatu hadi sita kukamilika
kwakwe na zitagharamiwa na fedha za ndani za Serikali ambapo ujenzi wake
unatarajiwa kuanza Desemba mwaka huu.
“Wataalamu
wanaendelea kubaini maeneo yatakayojengwa fly over hizo ikiwemo eneo la
Mwenge ambalo tayari wataalamu wamekubali kujenga fly over moja ya
magari”, amesema Prof. Mbarawa.
Hatua
hiyo ni mkakati wa Serikali kupunguza msongamano wa magari jijini Dar
es Salaam unaogharimu fedha nyingi kutokana na watu kupoteza muda mwingi
barabarani.
Katika
hatua nyingine Waziri Prof. Mbarawa amekagua maendeleo ya utoaji huduma
katika Daraja la Nyerere na kuagiza vitengenezwe vitambulisho vya msimu
vitakavyowawezesha watumiaji wa daraja kulipa tozo kwa miezi sita au
mwaka ili kupunguza msongamano wa kulipa kila siku.
“Hakikisheni
mnatengeneza na kuuza kadi za kuvukia katika daraja sehemu mbalimbali
ili kuwawezesha watumiaji kupata huduma hiyo kabla ya kufika darajani”, amesema Prof. Mbarawa.
Aidha
amemtaka Mtendaji Mkuu wa Daraja la Nyerere Bw. Gerald Sondo
kuhakikisha tozo zinakusanywa inavyostahili na kupanga njia maalumu za
kupita magari makubwa na madogo ili kuwezesha huduma ya kupita darajani
iwe ya haraka.
“Magari
yote yanayopita katika daraja hili yakiwemo ya Serikali ni lazima
yalipe tozo inayostahili isipokuwa yale yenye vibali maalumu yakiwemo ya
Jeshi la Wananchi, Zimamoto, Polisi, na yanayobeba wagonjwa
(Ambulance)”, amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.
Waziri
Mbarawa amesisitiza umuhimu wa wananchi kutunza na kulilinda Daraja
hilo ili lidumu kwa muda mrefu na kusisitiza adhabu kali kwa wataohujumu
miundombinu yake.
Naye
Mtendaji Mkuu wa Daraja la Nyerere Bw. Gerald Sondo amemueleza Waziri
Mbarawa kuwa chanagamoto zinazowakabili kwa sasa ni kubaini magari yenye
vibali maalumu, malalamiko ya magari ya abiria (daladala), uelewa mdogo
wa matumizi ya daraja na mazoea ya kupita bila ya kulipa tozo.
Zaidi
ya magari elfu nane hadi elfu kumi na tatu hupita katika daraja hilo
kwa siku huku watembea kwa miguu, baiskeli wakipita bila kulipa tozo.
Meneja
Mradi wa Daraja la Nyerere kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF),
Eng. Karim Mattaka, akitoa maelezo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa (kushoto), wakati alipotembelea daraja
hilo leo jijini Dar es salaam.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa (kulia),
akitoka kukagua moja ya Ofisi zilizopo katika daraja la Nyerere. Kushoto
ni Msimamizi wa daraja hilo kutoka NSSF Gerald Sondo.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa (kulia),
akipata maelezo ya ujenzi wa bomba la kupima mafuta (flow meter) kutoka
kwa Fundi mitambo wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Simon Dottto
(kushoto).
0 comments:
Post a Comment