TANZANA
kwa sasa inajikita zaidi katika utafiti wa madini yanayohitajika zaidi
duniani yakiwemo yanayotumika kutengeneza vifaa vya simu na betri za
magari, Bunge linaloendelea na vikao vyake mjini Dodoma limeambiwa.
Aidha
katika juhudi hizo, madini aina ya helium (he) yanayotumika kwa ajili
ya mitambo ya Apollo na pia kutumika kwenye vifaa vya matibabu kama MRI
na NMR yamegundulika kuwepo nchini Tanzania.
Akijibu
maswali ya wabunge jana, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
Muhongo, alisema kwamba baadhi ya madini kama chuma na shaba,
uhitajikaji wake duniani umepungua sana kwa sasa.
Katika
maswali yao, Mbunge wa Igunga (CCM), Dalaly Kafumu alitaka
kuthibitishiwa kuhusu uwepo wa taarifa kwamba utafiti wa madini nchini
mwetu umepungua sana.
Akijibu
swali hilo, Profesa Muhongo alitoa ufafanuzi kwamba madini yamekuwa
yakitafutwa kwa vipindi na yanapokuwa mengi, uhitajikaji wake hupungua
sambamba na utafiti.
Alifafanua kwamba katika miaka hii uhitaji wa baadhi ya madini kama shaba na chuma umepungua sana.
“Ndio
maana utaona hata uchumi wa Zambia umeyumba kwa sababu China ambayo
ndio mnunuzi mkubwa wa shaba kutoka nchini humo imepunguza mahitaji ya
madini hayo,” alisema Muhongo.
Alisema
madini yanayotengeza vifaa vya simu (rare earth mineral) na yale
yanayotengeza betri (graphite) yataendelea kutafutwa kila mara kutokana
na uhitajikaji wake na ndio maana akasema Tanzania nayo inajikita zaidi
katika kusaka madini hayo.
Alifafanua
kwamba madini hayo yanayotengeneza betri za magari yataendelea
kuhitajika sana kwa sababu ulimwengu wa sasa unajikita zaidi katika
kutengeneza magari yanayotumia umeme kwa wingi.
Kuhusu
madini ya helium ambayo huwa katika mfumo wa gesi inayopatikana katika
kina kifupi, Waziri Muhongo alifafanua kwamba utafiti ulifanywa na vyuo
vikuu vya Oxford na Durham ulithibitisha kwamba kuna madini hayo nchini.
Alifafanua
kwamba kiwango kilichogunduliwa cha madini hayo katika Ziwa Rukwa ni
mita za ujazo bilioni 52.2 na kwamba utafiti zaidi unaendelea. Kwa sasa
nchi inayozalisha kwa wingi madini hayo ni Marekani ambako hata hivyo,
Profesa Muhongo, alisema yamekuwa yakipungua siku hata siku.
0 comments:
Post a Comment