Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amelitaka
Jeshi la Polisi nchini na ofisi ya mwendesha mashitaka kujirekebisha kwa
kutekeleza wajibu wao huku wakitanguliza maslahi ya Taifa.
Rais Magufuli ametoa maagizo hayo leo tarehe 29 aprili, 2016 wakati
akifungua kikao cha kazi cha Makamanda wa Polisi wa Mikoa, Mawakili
wafawidhi wa serikali wa mikoa na wakuu wa upelelezi wa mikoa na vikosi,
kinachofanyika kwa siku mbili katika ukumbi wa mikutano wa Dodoma
uliopo katika eneo la Tambukareli mjini Dodoma.
Awali kabla ya kutoa hotuba yake Rais Magufuli aliwapa nafasi
Makamanda na mawakili wafawidhi hao kutoa maoni yao juu ya changamoto
zinazowakabili katika kutekeleza wajibu wa kufanya upepelezi na
kuendesha mashitaka, hususani kujua sababu za kuchelewesha kesi za
makosa ya jinai, ambapo wamedai ufinyu wa bajeti ndio sababu kubwa ya
kucheleweshwa kwa kesi za hizo.
Kufuatia kutajwa kwa changamoto hiyo Rais Magufuli ameahidi
kuhakikisha anawatafutia fedha kwa ajili ya kukabiliana nazo, lakini
ametaka fedha zitakazotafutwa zitumike vizuri kwa kuwa taarifa
zinaonesha Jeshi la Polisi limekuwa likihusishwa na matumizi mabaya ya
fedha hali inayoongeza ukubwa wa matatizo yanayokwamisha utendaji wake
wa kazi.
Ametolea mfano wa taarifa za matumizi mabaya ya fedha zinazotolewa
kwa ajili ya kununulia vifaa na sare za askari, ama mikataba yenye
mashaka inayotiwa saini kati ya Polisi na wawekezaji kuwa ni baadhi ya
mambo yanayoongeza hali ngumu ya utendaji kazi kwa jeshi hilo.
"Osterbay pale ni eneo ambalo ni very prime, kila mmoja anajua,
mmeingia kwenye mikataba mnayoijua nyinyi, akapewa mtu anawajengea pale,
sifahamu kama majengo hayo yanafaa. Palikuwa na ubaya gani eneo la
Osterbay likawa na hati, mkaitumia hiyo hati kwenda kukopa benki na
kujenga nyumba hata za ghorofa 20 pale, mkaweka investment na Polisi
wenu wakakaa pale. Nimesema lazima nizungumze kwa uwazi, nisiposema kwa
uwazi nitajisikia vibaya nikimaliza mkutano huu, nataka muelewe na
muelewe ukweli direction ninayoitaka mimi" amesema Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli ameitaka ofisi ya mwendesha mashitaka
kujipanga kufanya kazi kwa ufanisi na ameelezea kusikitishwa kwake na
vitendo vya serikali kushindwa katika kesi nyingi mahakamani licha ya
kuwa na wanasheria mahiri.
"Niwaombe mawakili na polisi wanaohusika na upelelezi mtangulize
maslai ya nchi mbele, kwa sababu kumekuwa na usemi kwa baadhi ya
wapelelezi na mawakili wachache,nasema wachache, panapokuwa na kesi
inayohusiana na pesa pesa,wana misemo yao wanasema dili limepatikana, na
saa nyingine kesi inapopelekwa mahakamani wana-collude mawakili wa
serikali na mawakili wanaomtetea mhalifu, na wanapo-collude siku zote
serikali inashindwa. Unapoona hali hiyo ya kila siku serikali
inashindwa, halafu siku hiyo unataka serikali ikuwezeshe, kwa vyovyote
serikali inapata kigugumizi" amesisitiza Rais Magufuli.
Dkt. Magufuli pia amelitaka Jeshi la Polisi kujiepusha na kashfa
ambazo zimekuwa zikisemwa dhidi yake, ikiwemo maafisa wa polisi
kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya na kuazimisha silaha kwa
wahalifu wa ujambazi.
Hata hivyo Rais Magufuli amelipongeza jeshi la Polisi na Ofisi ya
Mkurugenzi wa mashitaka kwa kazi kubwa wanayoifanya na ametaka apelekewe
mpango wa mahitaji yao ili atafute namna ya kuimarisha vyombo hivyo
0 comments:
Post a Comment